logo

TAMISEMI

Students

FR
Fred Kibanofred.kibano@tamisemi.go.tz

NIMESAINI NOTISI ZA KUVUNJA MABARAZA YA MADIWANI - MCHENGERWA

Na. James K. Mwanamyoto OR-TAMISEMI

Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais-TAMISEMI, Mhe. Mohamed Mchengerwa amesema kwa kuzingatia mamlaka aliyopewa kwa mujibu wa sheria, tayari amekwisha saini notisi za kuvunjwa kwa Mabaraza ya Madiwani katika Mamlaka za Wilaya na Mamlaka za Miji, kuelekea Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2025.

Waziri Mchengerwa amesema hayo leo, wakati akizungumza na waandishi wa habari katika Ukumbi wa Mikutano wa Ofisi ya Rais-TAMISEMI jijini Dodoma.

Mhe. Mchengerwa amesema kuwa, notisi hizo za Kuvunjwa kwa Mabaraza ya Madiwani katika Mamlaka za Wilaya, na Mamlaka za Miji, 2025 zitatangazwa kwenye Gazeti la Serikali hivi karibuni.

Mhe. Mchengerwa amefafanua kuwa, notisi hizo zinaelekeza kwamba vikao vya Halmashauri na Kamati zake zinapaswa ziwe zimekoma siku saba kabla ya kuvunjwa kwa Bunge hapo tarehe 27 Juni, 2025.

“Vikao vya Halmashauri na Kamati zake zinapaswa kuwa zimekoma ifikapo tarehe 20 Juni, 2025 hivyo Mkurugenzi wa Halmashauri atawajibika kwa kufanya kikao chochote cha Halmashauri au Kamati yake baada ya tarehe hiyo,” Waziri Mchengerwa amesisitiza.

Baada ya mabaraza ya madiwani kufikia ukomo tarehe 20 Juni 2025, Mhe. Mchengerwa ameelekeza masuala yote ya kiutendaji katika Halmashauri kusimamiwa na Mkurugenzi wa Halmashauri, ambaye atakuwa Mwenyekiti wa Halmashauri kwa kipindi cha mpito, akisaidiana na Wakuu wa Idara watakaokuwa kama wajumbe wa kamati.

Sanjari na hilo, Waziri Mchengerwa ameelekeza kuwa Mkurugenzi wa Halmashauri hataruhusiwa kuanzisha miradi au uwekezaji mpya ikiwa ni pamoja na kubadilisha au kurekebisha mradi, uwekezaji au uamuzi wowote uliopitishwa na Halmashauri kabla     ya kuvunjwa.

“Matumizi mabaya ya mamlaka au kutotekeleza kwa ufanisi majukumu ya kiutawala kwa mujibu wa notisi hizi, kutamfanya Mkurugenzi kuwajibika binafsi kwa mujibu wa Sheria,” Mhe. Mchengerwa amehimiza.

Pia, Waziri Mchengerwa ameelekeza kwamba katika kikao cha kwanza cha Baraza jipya la Madiwani baada ya uchaguzi kufanyika, Mkurugenzi wa Halmashauri atapaswa kuwasilisha taarifa ya     maamuzi na mwenendo wa vikao vya menejimenti     vilivyofanyika wakati wa kipindi cha mpito.

Aidha, Waziri Mchengerwa amewashukuru na kuwapongeza Madiwani wote waliomaliza muda wao wa uongozi kwa kutoa mchango mkubwa katika maendeleo ya Mamlaka za Serikali za Mitaa nchini.

Comments

Please sign in to leave a comment.

Matangazo Muhimu

Soma matangazo na taarifa rasmi ili kuendelea kufahamu shughuli zinazotekelezwa na Wizara.

Habari na Matukio

Soma matangazo na taarifa rasmi ili kuendelea kufahamu shughuli zinazotekelezwa na Wizara.

Cookie

We use cookies to enhance your browsing experience, provide personalized content, and analyze our traffic. By clicking "Accept All Cookies", you agree to the storing of cookies on your device to improve site navigation, analyze site usage, and assist in our marketing efforts. To learn more about how we use cookies and to manage your preferences, please visit our Cookie Policy.
National Election Commission Logo

Uchaguzi 2025

Kujiandikisha Kuwa Mpiga Kura ni Msingi wa Uchaguzi Bora