
WASIMAMIZI WA MRADI WA SHULE HATARINI, MKUU WA MKOA AAGIZWA KUWAKAMATA NA KUWAHOJI
Mkuu wa Mkoa wa Mtwara Mhe. Kanali Patrick Sawala ameagizwa kuwakamata na kuwahoji wahusika wa usimamizi wa mradi wa Shule ya Sekondari ya Amali Makondeni, iliyopo Halmashauri ya Wilaya ya Tandahimba, kufuatia tuhuma za usimamizi mbovu wa mradi huo.
Maelekezo hayo yametolewa na Naibu Waziri wa Ofisi ya Waziri Mkuu, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (OWM–TAMISEMI) anayeshughulikia Elimu, Mhe. Reuben Kwagilwa, kwa niaba ya Waziri wa Nchi OWM–TAMISEMI, Mhe. Profesa Riziki Shemdoe mara baada ya kukagua utekelezaji wa mradi huo.
Mhe. Kwagilwa amesema mradi huo umetumia zaidi ya shilingi milioni 464 bila kukamilika huku ukihitaji shilingi milioni 48 zaidi kwa ajili ya ukamilishaji, hali aliyoitaja kuwa ni kinyume na maelekezo ya Serikali na inaashiria uzembe na upotevu wa fedha za umma.
“Ninamwelekeza Mkuu wa Mkoa kufuata taratibu za kisheria na kutumia mamlaka aliyonayo kuwakamata na kuwahoji wahusika wa mradi huu kwa tuhuma za upotevu wa shilingi milioni 48,” amesema Mhe. Kwagilwa.
Baada ya kubaini dosari za kiusimamizi katika mradi huo, Naibu Waziri huyo pia amemuagiza Katibu Mkuu wa OWM–TAMISEMI kuhakikisha ndani ya siku 21 anapelekwa Mkuu wa Idara ya Ujenzi katika halmashauri husika ili kuboresha usimamizi na kuongeza ufanisi katika utekelezaji wa miradi ya maendeleo.
Comments
Join the conversation
Please sign in to share your thoughts and interact with the community.

