
SERIKALI YAIMARISHA MATUMIZI YA MFUMO WA SIS KATIKA USIMAMIZI WA ELIMU NCHINI
Serikali kupitia Ofisi ya Waziri Mkuu - TAMISEMI imetangaza maboresho makubwa katika Mfumo wa Taarifa za Shule (School Information System - SIS) kwa kuunganisha mifumo mbalimbali ya kisekta ili kuimarisha uwazi na upatikanaji wa takwimu sahihi za elimu nchini.
Hatua hiyo imekuja kufuatia maelekezo ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan, aliyetoa mwongozo mwezi Aprili 2024 akitaka mifumo ya Serikali isomane ili kuondoa urasimu na utitiri wa mifumo inayohitaji taarifa zinazofafana katika ngazi ya shule.
Akifungua mafunzo ya siku nne kwa Maafisa Taaluma, Maafisa Elimu Vifaa na Takwimu, pamoja na Maafisa TEHAMA mkoani Tabora, Naibu Katibu Mkuu, Ndugu Atupele Mwambene, amebainisha kuwa mfumo huo ulioboreshwa sasa unajumuisha mifumo mingine muhimu kama Mfumo wa Uthibiti Ubora wa Shule (SQA MIS), Mfumo wa Usajili wa Shule (SAS), PReM, PReMs, TSC MIS na Mwalimu DataLake MIS
“Lengo kuu la kuunganisha mifumo hii ni kuhakikisha kuwa Serikali inapata taarifa za elimu kupitia jukwaa moja, jambo litakalosaidia kufanya maamuzi sahihi ya kisekta na kupanga mipango ya maendeleo kwa ufanisi zaidi kulingana na mahitaji halisi ya shule nchini.” Amesema ndugu Atupele
Katika mabadiliko hayo makubwa, Ameelekeza kuwa, kuanzia mwaka 2026, mfumo wa SIS uanze kutumika rasmi katika michakato ya kujiunga na masomo kwa kuwapatia wadau fomu za maombi ya kujiunga na Kidato cha Kwanza (TSM 9), fomu za kujiunga na Kidato cha Tano (Selform) pamoja na takwimu zitakazotumika kwenye utoaji wa fedha za ruzuku kwa shule kila mwezi.
Pamoja na mafanikio yaliyopatikana katika uhuishaji wa taarifa za walimu ambapo utekelezaji umefikia wastani wa asilimia 85 kwa shule za msingi za serikali na asilimia 89 kwa sekondari, Naibu Katibu Mkuu ameelezea kutoridhishwa kwake na baadhi ya mikoa na halmashauri ambazo bado zinasuasua.
“Takwimu zinaonesha kuwa baadhi ya shule za binafsi bado ziko nyuma kwa asilimia 48, huku halmashauri kama Mafinga, Moshi DC, na Namtumbo zikiwa chini ya asilimia 50. Hali hii imeipelekea TAMISEMI kutangaza kuwa kuanzia sasa, matumizi ya mifumo ya kielektroniki ikiwemo SIS yatatumika kama kigezo cha kupima utendaji kazi wa maafisa elimu na wasimamizi wa sekta hiyo katika ngazi za mikoa na halmashauri.” Amesema ndugu Atupele
Kwa upande wake, Mratibu msaidizi wa program ya BOOST na msimamizi wa mfumo wa taarifa za shule (SIS) Bwana Reuben Swilla amesema kuwa lengo la mafunzo haya ni kuwezesha upatikanaji wa takwimu sahihi na taarifa sahihi za shule kwa wakati sahihi katika shule zote za msingi Tanzania bara
Comments
Join the conversation
Please sign in to share your thoughts and interact with the community.

