
WAKURUGENZI WA HALMASHAURI WATAKIWA KUTENGA RASILIMALI ZA KUTOSHA KULINGANA NA MAHITAJI YA WATOTO
Katibu Mkuu Ofisi ya Waziri Mkuu – TAMISEMI, Adolf Ndunguru, amewataka Wakurugenzi wa Halmashauri kutenga rasilimali za kutosha kwa ajili ya utekelezaji wa afua mbalimbali za malezi, makuzi na maendeleo ya mtoto kulingana na mahitaji ya watoto katika maeneo yao.
Katika hotuba yake ya ufunguzi wa mafunzo ya siku tatu kwa Maafisa Ustawi wa Jamii kutoka Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa juu ya matumizi ya kadi ya alama (scorecard), Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum, Wakili Amon Mpanju, kwa niaba ya Katibu Mkuu Ndunguru amesisitiza Wakurugenzi kutenga fedha kama rasimali muhimu kuwezesha utekelezaji wa programu jumuishi ya taifa ya malezi, makuzi na maendeleo ya awali ya mtoto.
Awali akimkaribisha mgeni rasmi Mkurugenzi Msaidizi wa huduma za Ustawi wa Jamii kutoka Ofisi ya Waziri Mkuu TAMISEMI Bi. Subisya Kabuje amesema kadi hiyo ya alama (Scorecard) itawasaidia maafisa ustawi wa jamii na wataalamu mbalimbali katika ngazi ya halmashauri, kupata takwimu sahihi zitakazotumiwa na serikali katika kufanya maamuzi mbalimbali kwa ajili ya matokeo chanya katika ngazi ya jamii.
Kwa mujibu wa Mkurugenzi wa shirika la TECDEN ambao ni wadau walioshiriki kuandaa kadi hiyo ya alama, Mwajuma Kibwana, pamoja na faida zingine itasaidia kwenye mipango ya kibajeti na kisera katika kuhakikisha mamlaka za Serikali za Mitaa zinajipima katika uboreshaji wa utoaji wa huduma za malezi, makuzi na maendeleo ya awali ya mtoto kwa kutumia viashiria 14 kutoka kwenye maeneo matano ambayo ni Afya bora, Ujifunzaji wa awali, Malezi yenye mwitikio, Lishe toshelevu, Ulinzi na Usalama.
“Kadi hiyo ya alama inachagiza utekelezaji wa programu jumuishi ya taifa ya malezi, makuzi na maendeleo ya awali ya mtoto na imetengenezwa na watanzania kwa kuzingatia mahitaji ya watanzania, hivyo sisi kama wadau wa watoto tunahamasisha na kusisitiza matumizi sahihii ya taarifa katika ngazi mbalimbali kwa maslahi ya watoto ili siku moja wote tujivunie kuwa waasisi wa kadi hiyo ya alama nchini” alisema Bi Kibwana.
Mafunzo hayo ya siku tatu yanayofanyika Mkoani Morogoro yamewashirkisha Maafisa Ustawi wa Jamii zaidi ya 200 kutoka Halmashauri zote 184 na Mikoa 26 ya Tanzania bara yakilenga kuwajengea uwezo wataalamu hao juu ya matumizi sahihi ya kadi ya alama (Scorecard) ili kubaini viashiria vya malezi, makuzi na maendeleo ya awali ya mtoto mwenye umri wa miaka 0–8, ili kusaidia Watoto kufikia ukuaji timilifu.
Comments
Please sign in to leave a comment.

