
WAGANGA WAKUU WA MIKOA WAAGIZWA KUSIMAMIA MAADILI NA WELEDI KATIKA SEKTA YA AFYA
Naibu Katibu Mkuu, Ofisi ya Waziri Mkuu – TAMISEMI anayeshughulikia Afya, Prof. Tumaini Nagu, amewataka Waganga Wakuu wa Mikoa (RMOs) kusimamia maadili na weledi wa watumishi wa sekta ya afya kwa kuzingatia misingi na taaluma ya fani hiyo.
Prof. Nagu alitoa maelekezo hayo wakati akifunga kikao kazi cha kutathmini utoaji wa huduma za UKIMWI, Kifua Kikuu (TB), Malaria na huduma unganishi za afya, kilichowakutanisha Waganga Wakuu wa Mikoa, Wafamasia wa Mikoa, Waratibu wa UKIMWI na Waratibu wa Malaria kilichofanyika Jijini Dodoma.
“Ni jukumu letu kama wasimamizi kuhakikisha watumishi wa sekta ya afya wanazingatia taaluma na misingi ya kazi zetu. Tusimame kwenye weledi na maadili katika maeneo yetu yote,” amesema Prof. Nagu.
Amesema kuwa kwa miaka mingi sekta ya afya imekuwa miongoni mwa tasnia zenye heshima na zinazoaminika katika jamii, hivyo ni muhimu kurejesha na kuendeleza misingi hiyo ili kulinda imani ya wananchi kwa watoa huduma.
Pia, Prof. Nagu amewataka Waganga Wakuu wa Mikoa (RMOs) kusimamia kikamilifu usalama wa vifaa na vifaa tiba katika vituo vya kutolea huduma za afya ngazi ya msingi.
“Tulishatoa maelekezo kuhakikisha vifaa na vifaa tiba vyote vinasimamiwa na kuwekwa mifumo ya usalama ili kuepusha upotevu. Vifaa hivi vina gharama kubwa zaidi kuliko mifumo inayotakiwa kuwekwa,” amesisitiza.
Kwa upande wake, Mkurugenzi wa Idara ya Afya, Lishe na Ustawi wa Jamii, Dkt. Rashid Mfaume, amewataka washiriki wa kikao hicho kuhakikisha wanatekeleza kwa vitendo maazimio yote waliyokubaliana ili kuboresha utoaji wa huduma kwa wananchi.
Comments
Please sign in to leave a comment.

