
PROF. NAGU AHAMASISHA WANANCHI KUJIUNGA NA BIMA YA AFYA KWA WOTE
Naibu Katibu Mkuu Ofisi ya Waziri Mkuu TAMISEMI (AFYA) Prof. Tumaini Nagu amewaasa wananchi kujiunga na Bima ya Afya kwa Wote ili kuwa na uhakika wa huduma za afya wakati wowote bila changamoto ya kifedha.
Prof. Nagu ametoa rai hiyo wakati akisalimiana na wananchi waliokuwa wakipatiwa huduma katika hospitali ya Halmashauri ya Wilaya ya Mlimba. wakati akiendelea na ziara yake ya usimamizi shirikishi kwa kuangalia upatikanaji wa Huduma za Afya, Lishe na Ustawi wa Jamii katika Halmashauri hiyo.
“Huduma za Afya ni gharama na nilazima huduma hizi ziwe endelevu, ili wewe mwananchi upate huduma wakati wowote ni vyema tukapata Bima ya Afya, Bima ya Afya Kwa Wote itakuwa itasaidia Wananchi kupata huduma wakati wowote bila changamoto ya kifedha” amesisitiza Prof. Nagu.
Aidha, Prof. Nagu amewakumbusha watumishi katika Sekta ya Afya nchini kuhakikisha wanakuwa waadilifu na waaminifu kwa viapo vyao vya kuhudumia wagonjwa.
“Tuna viapo ambavyo tumeviapa mbele ya wahudumu wetu, mbele ya wale waliotusimamia na kutufundisha lakini viapo vile ni kati yetu sisi na Mungu hivyo yafaa kuviishi na kuwa waaminifu” alisema Nagu.
Pia. Prof. Nagu amempongeza Mkurugenzi wa Halmashauri ya Mlimba Ndug. Jamary Idrisa Abdul kwa kufanikisha ujenzi wa nyumba za kisasa za watumishi wa hospitali ya Halmashauri kwani inawapa moyo watumishi wake na kurahisisha upatikanaji wa huduma za afya kwa kuwepo maeneo ya karibu na Halmashauri.
Naibu Katibu Mkuu ameanza ziara yake ya usimamizi shirikishi katika Mkoa wa Morogoro ambapo atatembelea katika Halmashauri za Wilaya Mlimba, Ulanga, Malinyi na Halmashauri ya Mji wa Ifakara.
Comments
Please sign in to leave a comment.

