Benki ya dunia kutumia dola milioni 130 katika Miradi ya TSCP

Mathew Kwembe

Benki ya dunia kutumia dola milioni 130 katika Miradi ya TSCP

Serikali imeishukuru benki ya dunia kwa kukubali kutoa kiasi cha dola za marekani milioni 130 kugharamia awamu ya pili ya utekelezaji wa mradi wa uendelezaji miji ya kimkakati (TSCP).

Aidha Serikali pia imelipongeza shirika la maendeleo la Denmark DANIDA kwa kutoa kiasi cha dola za marekani milioni 22.5 kwa ajili ya kuimarisha mifumo ya ukusanyaji mapato, mifumo ya utambuzi na ukusanyaji taarifa katika Mamlaka hizo za Serikali za Mitaa.

Akifungua Mkutano wa kujadili taarifa ya robo mwaka ya utekelezaji wa Mradi huo ambao unapata fedha kutoka benki ya Dunia na Shirika la Maendeleo la Denmark DANIDA jana mjini Mtwara, Katibu Mkuu Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa Mhandisi Mussa Iyombe alizitaka Mamlaka za Serikali za Mitaa zinazotekeleza mradi huo katika awamu hii ya pili kuwa tayari kutekeleza kwa ufanisi, ili iwe na mafanikio zaidi.

Katika hotuba yake ambayo ilisomwa na Katibu Tawala wa Mkoa wa Mtwara bwana Alfred Luanda Katibu Mkuu alisema kuwa katika kipindi cha miaka 6 cha utekelezaji wa mradi wa uendelezaji miji ya kimkakati, kumekuwa na mafanikio kadhaa yanayoonekana yaliyotokana na utekelezaji wa mradi huo kama vile halmashauri hizo kupatiwa magari pamoja na vifaa vya kukusanyia taka ngumu, ujenzi wa barabara kwa kiwango cha lami katika miji hiyo, uchimbaji mitaro ya maji taka pamoja na ujenzi wa maeneo ya kuhifadhia taka.

Alisema pia Mamlaka za Serikali za Mitaa zilipata fursa ya kusimika mifumo ya kijiografia ya utambuzi (GIS), mifumo ya ukusanyaji mapato (LGRCIS) na Mifumo ya SOMMA), ambayo kwa kiasi kikubwa imechochea maendeleo katika mamlaka hizo za serikali za Mitaa.

Hata hivyo Katibu Mkuu amezishauri Mamlaka za Serikali za mitaa kutenga fedha zitokanazo na mapato yao ya ndani kwa ajili ya kuhakikisha kuwa zinatumika kwa ajili ya kufanyia matengenezo magari pamoja na miundo mbinu ya mradi ili iwe endelevu.

“Nazitaka Mamlaka zote za Serikali za Mitaa zinazotekeleza mradi huu kujenga tabia ya kutenga kiasi cha fedha cha kutosha katika bajeti zao za mapato ya ndani kwa ajili ya kufanyia ukarabati miundombinu na vifaa vilivyonunuliwa na mradi huu,” alisema Katibu Mkuu.

Kwa upande wa miradi iliyokuwa inapata fedha kutoka DANIDA, Katibu Mkuu alisema kuwa miradi hiyo imesaidia sana kuimarisha halmashauri hizo hasa kwa kuzipatia ujuzi, vifaa vya kufanyia kazi na kuimarisha mifumo ya kama ile ya ukusanyaji mapato, Mifumo ya kijiografia, mifumo ya utambuzi wa mafaili pamoja na ongezeko la mapato na ukusanyaji wa taarifa mbalimbali za halmashauri.

Katibu Mkuu alisifu pia miradi hiyo iliyo chini ya DANIDA kwa kuja na mikakati ya kuweka kipengele cha fedha za matengenezo kwani hatua hiyo itasaidia sana katika kuifanya miradi hiyo kudumu na kuwa endelevu.

Alisema pia Mamlaka za Serikali za Mitaa zilipata fursa ya kusimika mifumo ya kijiografia ya utambuzi (GIS), mifumo ya ukusanyaji mapato (LGRCIS) na Mifumo ya SOMMA), ambayo kwa kiasi kikubwa imechochea maendeleo katika mamlaka hizo za serikali za Mitaa.

Alisema kuwa ili miundombinu hiyo iwe endelevu mamlaka za Serikali za Mitaa zitapaswa kutenga fedha katika bajeti zao kama alivyoagiza Katibu Mkuu Ofisi ya Rais Tamisemi ili kiasi hicho kitumike kwa ajili ya kufanyia ukarabati vifaa na miundo mbinu husika.

"Kupitia mradi huu, halmashauri hizi tumezipa vifaa kama vile magari ya kukusanyia taka, miundombinu ya barabara, na kujenga mitaro ya barabara, hivyo halmashauri hazina budi kutenga fedha ili waweze kusafisha mitaro na kukarabati barabara ili miundombinu hii iweze kudumu," alisema.

Naye Mhandisi Barnabas Faida kutoka Manispaa ya Dodoma alisema kuwa agizo la Katibu Mkuu linatekelezeka kwani tayari Serikali ilikwishaagiza kuwa kila halmashauri inapaswa kutenga asilimia 60 ya mapato yake ya ndani kwa ajili ya kushughulikia miradi ya maendeleo kwa hiyo, suala hili linatekelezeka.

Alisema kuwa jambo muhimu ni kwa maafisa masuuli katika mamlaka za Serikali za Mitaa kuzingatia agizo hilo la serikali na kuhakikisha kuwa kiasi hicho cha asilimia 60 kinatumika kwa ajili ya miradi ya maendeleo.

Kikao cha kujadili ripoti ya robo mwaka kinawashirikisha wadau mbalimbali kutoka Benki ya dunia, shirika la Maendeleo la Denmark DANIDA, Ofisi ya Rais TAMISEMI, Wizara ya Fedha, Ofisi ya Makamu wa Rais- Mazingira pamoja na halmashauri 9 zinazotekeleza mradi huo.

Mradi wa Uboreshaji wa miundombinu mijini unatekelezwa katika halmashauri za miji ya Arusha, Dodoma, Mwanza, Mbeya, Kigoma Ujiji, Tanga, na Mtwara Mikindani. Mradi huu ulizinduliwa mwezi septemba mwaka 2010 na awamu ya pili ya utekelezaji wa mradi huu inatarajiwa kuanza julai, 2017.

INFORMATION
Vigezo vya uanzishaji na upandishaji hadhi wa mamlaka za serikali za mitaa
Taratibu za kupandishwa vyeo na mafunzo kwa watumishi wa MSM
Utaratibu wa Jinsi ya Kushughulikia Malalamiko Serikalini.
Maelezo kuhusu utaratibu wa uhamisho kwa watumishi wa Umma
Majukumu Na kazi za Meya,Madiwani,Wenyeviti wa Vijiji na Vitongoji.
EVENTS
SIGN UP

COUNTER STARTED ON:27th July 2015.