Wazazi watakaoshindwa kupeleka watoto shule kuchukuliwa hatua

Na.Shani Amanzi na Mwajuma Ally

Wazazi watakaoshindwa kupeleka watoto shule kuchukuliwa hatua

Serikali imewaagiza Wakuu wa wilaya kuhakikisha wanawachukulia hatua za kisheria wazazi watakaoshindwa kuwapeleka shule watoto wao waliochaguliwa kujiunga na kidato cha kwanza kwa kuwapa kazi ya kuendesha bodaboda.

Agizo hilo limetolewa jana na Naibu Waziri, Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa(Tamisemi), Mhe.Selemani Jafo alipofanya ziara ya kukagua miundombinu mbalimbali katika shule za msingi, Chadulu, Chang’ombe A na B, Manispaa ya Dodoma.

"Hatutaki mtoto akose elimu hasa katika kipindi hichi ambacho serikali imeamua kuelekeza nguvu za kutosha kwenye elimu kwa ajili ya watanzania.Kwa mzazi ambaye mtoto wake atabainika hajaenda shule na kupewa kazi zingine kama kuendesha bodaboda hatua za kisheria zichukuliwe mara moja,"alisema Mhe. Jafo

Alikemea tabia ya wazazi kutotilia mkazo masuala ya elimu na kuwakabidhi watoto wao kuendesha bodaboda kama ajira yao badala ya kuwapeleka shule.

"Kwa nchi zima watoto waliochaguliwa kujiounga na kidato cha kwanza wakuu wa wilaya hakikisheni wanaenda shule na wazazi ni wajibu wao kuwanunulia mahitaji yote ya shule kama sare za shule,"alisisitiza Naibu Waziri

Alisitiza serikali haitarajii kuna vijana waliochaguliwa wakishawishiwa na wazazi kufanya vibaya kwenye mitihani kutokana na elimu kuwa ni bure.

Akizungumzia kuhusu watoto walioandikishwa kuanza kusoma elimu ya awali na msingi, Mhe.Jafo alisema uandikishaji unaendelea vizuri na kuna idadi kubwa ya watoto wanaoandikishwa kwa sasa kutokana na elimu kuwa bure.

Hata hivyo, alisema kuna baadhi ya maeneo zimejitokeza changamoto kama zilivyojitokeza mwaka jana ambapo idadi ya watoto walioandikishwa imekuwa ni kubwa ukilinganisha na uwepo wa miundombinu.

"Kwa mfano Kagera kuna shule ipo Nyakanaza siku niliyofika kulikuwa na takribani wanafunzi wapya 800 wa darasa la kwanza, kwahiyo shule zilishazidiwa,"alisema Mhe.Jafo

Naibu Waziri huyo alibainisha shule nyingi idadi ya wanafunzi imeongezeka zaidi na kwa serikali ni faraja kuona watanzania wengi sasa wanapata elimu huku akiwataka wazazi wahakikishe watoto walioandikishwa wanahudhuria shule ipasavyo.

Kadhalika, Mhe.Jafo alisema ameridhishwa na ukarabati wa miundombinu mbalimbali kwenye shule hizo huku akiwaahidi walimu kuwa serikali itaendelea kuboresha mazingira ya kufundishia ili waweze kufanya kazi zao kwa ufanisi.

Kwa upande wake, Mkurugenzi wa Manispaa ya Dodoma, Godwin Kunambi, alisema kwa sasa Manispaa hiyo inaendelea kukabiliana na changamoto mbalimbali ikiwa ni pamoja ujenzi wa shule za msingi na sekondari na kuongeza madarasa kwenye baadhi ya shule ili kukabiliana na ongezeko la wanafunzi hasa wanaohamia Dodoma.

Naye, Ofisa Elimu wa Manispaa hiyo, Scholastika Kapinga, alisema hadi sasa watoto zaidi ya 8,000 wameandikishwa kwenye manispaa hiyo kuanza kusoma elimu ya awali na msingi.

INFORMATION
Vigezo vya uanzishaji na upandishaji hadhi wa mamlaka za serikali za mitaa
Taratibu za kupandishwa vyeo na mafunzo kwa watumishi wa MSM
Utaratibu wa Jinsi ya Kushughulikia Malalamiko Serikalini.
Maelezo kuhusu utaratibu wa uhamisho kwa watumishi wa Umma
Majukumu Na kazi za Meya,Madiwani,Wenyeviti wa Vijiji na Vitongoji.
EVENTS
SIGN UP

COUNTER STARTED ON:27th July 2015.